DHAHABU NYINGINE YAJA YANGA

Mshambuliaji wa Yanga Ibrahim Ajib jana kwa mara nyingine amedhihirisha ubora wake pale alipoifungia Yanga bao la pili la ushindi na kufanikiwa kuondoka na alama zote tatu ugenini dimba la Kaitaba.

Ajib pia ndiye aliyetengeneza bao la kwanza lililofungwa na Obrey Chirwa huku Chirwa nae akimtengenezea Ajib kufunga bao lake.

Wawili hao walionekana kuwa na ushirikiano mzuri katika mchezo wa jana, Hakika kama wakiendelea kuchezeshwa pamoja kuna kila uwezekano kuwa wataibeba Yanga.

Ajib kiwango chake kinazidi kuimarika tangu atue Yanga. Ameanza michezo yote ya VPL na kufanikiwa kufunga mabao matatu.

Huu ndio mguu wa dhahabu wa klabu ya Yanga kwani mara nyingi mabao yake yote aliyofunga yamepeleka ushindi Jangwani.

Naweza kusema pointi tisa kati ya 12 ilizopata Yanga zimepita mguuni kwa Ajib.

Kocha Mkuu George Lwandamina ameongeza kitu kwa Ajib. Wakati yuko Simba walikuwa wakisema ni 'mvivu' hajitumi anapokuwa uwanjani.

Lakini huyo sio Ajib wa Yanga. Huyu wa Yanga yuko fiti, anarudi chini kukaba inapolazimu na sio rahisi kumnyan'ganya mpira mguuni mwake.

Tayari ana mabao matatu, huyo Okwi mwenye mabao sita habari zimfikie, Ajib anakitaka kiatu cha dhahabu!

Maoni

Machapisho Maarufu