MAUAJI YA KINYAMA YATOKEA SINGIDA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
(PRESS RELEASE)
MAUAJI
Mnamo tarehe 08.09.2010 Huko katika Kituo cha Polisi Kinampanda, Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida Benard Shumba, (47), Mnyiramba, Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Yulansoni, Kata na Tarafa ya Kinyangiri, Wilaya ya Mkalama, Mkoani Singida alifika Kituoni hapo na kutoa taarifa kuwa Mke wake aitwaye Tabu Robert, (28), Mkazi waYulansoni haonikani nyumbani kwake. Juhudi za kumtafuta kwa kushirikiana na ndugu zake zilianza bila mafanikio ndipo alipoendelea kuishi kijijini hapo akitunza mwanae aliyeachwa na Mama yake.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Raia wema liliendelea kumtafuta bila mafanikio ambapo siku ya tarehe 17.03.2018 lilipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa Tabu Robert hakupotea bali aliuwa na Mme wake. Askari wa Jeshi la Polisi walifika nyumbani kwa Mtuhumiwa na kufanikiwa kumkamata ambapo alihojiwa na kukiri kufanya mauaji hayo siku ya tarehe 07.09.2010 majira ya saa 2:00 usiku akiwa nyumbani kwake na kukiri kuwa baada ya kutenda kosa hilo aliuchukua mwili wa Marehemu na kwenda kuuficha kwenye mti wa mbuyu ambao una shimo kubwa na kisha kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi hicho.
Uchunguzi wa Polisi umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ulevi wa pombe za kienyeji wa Marehemu na kumuacha Mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili peke yake kitendo ambacho kimekuwa kero kwa Mtuhumiwa.
Siku ya tarehe 18.03.2018 majira ya saa 10:00 jioni Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wananchi walifika eneo la tukio ambalo lipo umbali wa Mita 600 kutoka nyumbani kwa Mtuhumiwa na kukuta masalia ya mifupa, fuvu na mbavu zidhaniwazo kuwa ni za binadamu ndipo Polisi walipochuka sampuli za mabaki hayo kwa uchunguzi zaidi na mabaki mengine kukabidhiwa kwa Ndugu wa Marehemu kwa hatua za mzishi.
Kuhusiana na tukio hilo Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa Benard s/o Shumba kwa uchunguzi zaidi na baada ya uchunguzi kukamilika atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kutoa Wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa Taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahalifu katika maeneo yao ili kuzidi kutokomeza uhalifu Mkoani Singida pia kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi pindi wanapokuwa na migogoro ya aina yoyote bali watoe taarifa kwa viongozi wa Serikali za Mitaa au katika vituo vya Polisi vilivyokaribu na wao ili matatizo yao yatatuliwe kisheria.
.
Maoni
Chapisha Maoni