MOHAMMED RASHIDI KUTUA YANGA

Wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Jumatano ijayo, Novemba 15, tayari vigogo wa soka nchini wameanza kupigana vikumbo kusaka wachezaji wakali kuimarisha vikosi vyao.

Mshambuliaji wa Prisons Mohammed Rashidi tayari ameingia kwenye Radar za Yanga huku pia Azam FC nayo ikidaiwa kumnyemelea mshambuliaji huyo chipukizi mwenye umri wa miaka 22.

Rashidi ameuanza msimu huu kwa kishindo. Mpaka sasa tayari ameifungia Tanzania Prisons mabao sita akishika nafasi ya pili katika orodha ya vinara wa upachika mabao ligi kuu ya Vodacom.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zinabainisha kuwa inahitaji kusajili washambuliaji wawili katika jitihada za kuimarisha kikosi chake kilichoanza kwa kusuasua kwenye upachikaji mabao.

Washambuliaji pekee wanaotegemewa kwa sasa ni Obrey Chirwa na Ibrahim Ajib huku Donald Ngoma na Amissi Tambwe wakiwa majeruhi.

Ngoma hayupo kabisa nchini na ameingia katika mgogoro na viongozi wa Yanga baada ya kuondoka nchini bila ya ruhusa.

Tambwe hajacheza mchezo wowote msimu huu kutokana na majeruhi ya goti.

Yanga inakusudia kusajili mshambuliaji mmoja mzawa na mwingine wa Kimataifa kukiwa na uwezekano wa kuvunja mkataba wa mmoja wa washambulia hao.

Maoni

Machapisho Maarufu